DARAJA (Developing Risk Awareness through Joint Action) ni mradi unaolenga kuboresha upatikanaji na matumizi ya taarifa muhimu za hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi kwa wakazi wa makazi yasiyo rasmi (informal settlements) katika miji ya Dar es Salaam (Tanzania) na Nairobi (Kenya). Mradi huu utawawezesha wakazi kuwa na ustahimilivu zaidi na maandalizi bora ya kuchukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Aidha, mradi unalenga kuyawezesha Mamlaka za Jiji kufanya maamuzi bora yanayotegemea taarifa sahihi za hali ya hewa na tabianchi kuhusiana na makazi yasiyo rasmi ya mijini.

Mradi huu uko chini ya mpango wa Weather and Climate Information Services for Africa (WISER) – Afrika Mashariki, unaofadhiliwa na DFID na kusimamiwa na UK Met Office. Washirika wa utekelezaji ni CCI (Tanzania), KDI (Kenya) na Resurgence (Uingereza) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Idara ya Hali ya Hewa Kenya (KMD).

Malengo ya Mradi

  • Kuimarisha ustahimilivu wa watu wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi ya mijini kupitia ubunifu wa pamoja wa mifumo na huduma zinazolenga kukabiliana na hatari zinazohusiana na tabianchi.
  • Kupatikana kwa taarifa za tabianchi zilizoandaliwa kwa ushirikiano, zinazoaminika na kufikika kwa urahisi ili kusaidia maamuzi ya mipango katika ngazi ya jiji au makazi.
  • Kuongeza matumizi ya taarifa za tabianchi zilizoandaliwa kwa ushirikiano, zinazoaminika na zinazofikika miongoni mwa wakazi wa makazi yasiyo rasmi.

Vipengele vya Mradi wa Majaribio wa DARAJA

Mradi wa majaribio wa DARAJA ulikuwa na njia tatu za utoaji wa taarifa kama njia ya kuwezesha mawasiliano ya taarifa za hali ya hewa na tabianchi. Njia hizi zilitambuliwa kupitia taarifa zilizopatikana katika utafiti wa awali (baseline study) na ushirikishwaji wa wadau katika mchakato wa ubunifu wa pamoja (co-designing).

Njia ya Shule (School Channel)

Njia ya Shule inalenga kuhamasisha na kuendeleza uelewa kuhusu umuhimu wa taarifa za hali ya hewa na tabianchi. Wanafunzi kutoka shule mbalimbali hupatiwa mafunzo kupitia vilabu vya shule ili waweze kufasiri na kuwasilisha taarifa za hali ya hewa na tabianchi kwa wanafunzi wenzao pamoja na wazazi wao. Kupitia njia hii, wanafunzi huelimisha, kutoa taarifa na kuwahamasisha wazazi wao kuchukua hatua stahiki kulingana na utabiri wa hali ya hewa.

Shughuli hizi hufanyika kwa ushirikiano na msaada wa walimu wao, ambao pia wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu mawasiliano ya taarifa za hali ya hewa na tabianchi.

“Wanafunzi waliwafahamisha wazazi wao, hususan wale wanaoishi bondeni. Wazazi walitumia taarifa hizo kulinda mali zao ambazo awali zilikuwa zikiharibiwa na mafuriko, ikiwemo vitabu vya shule vya wanafunzi. Safari hii hali ilikuwa tofauti, kwani tahadhari zilichukuliwa mapema zaidi.”
Bi. Jane Brown – Shule ya Msingi Keko Mwanga

Njia ya Vyombo vya Habari (Media Channel)

Redio na Televisheni zilibainika kuwa njia zinazopendelewa kwa mawasiliano ya taarifa za hali ya hewa na tabianchi. Waandishi wa habari kutoka kwa washirika wa vyombo vya habari wa mradi wa DARAJA walipatiwa mafunzo ya kufasiri taarifa za hali ya hewa na tabianchi na kutoa ushauri unaohusiana na athari, pamoja na kutoa taarifa za mara kwa mara za utabiri wa hali ya hewa.


Njia ya Viongozi wa Mtaa na Vikundi vya Jamii

Viongozi wa mitaa kwa kushirikiana na Kamati za Maafa pamoja na viongozi wa vikundi vya jamii hupatiwa mafunzo ya kufasiri utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). Mfumo wa mawasiliano ya kijamii umeanzishwa ambapo viongozi wa jamii waliopatiwa mafunzo husambaza utabiri wa hali ya hewa wa kila wiki na tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa kutumia lugha rahisi kueleweka.

Taarifa hizi husambazwa kupitia mlolongo wa ujumbe unaowafikia wanajamii kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu (SMS) au kwa mawasiliano ya ana kwa ana (maneno ya mdomo).